Kenya yakanusha madai ya kupora Somalia

Image caption Makaa katika Bandari ya Kismayo

Jeshi la Kenya limekanusha madai kuwa limekuwa likipora raslimali ya Somalia kwa kuhusika na uuzaji wa makaa katika mji wa bandari wa Kismayo.

Ripoti ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa inaishtumu jeshi la Kenya kwa kuuza makaa nje ya Somalia kinyume na sheria katika Bandari hiyo ya Kisimayo.

Kamati kuu ya usalama ya Umoja wa Mataifa ilikuwa imepiga marufuku uuzaji wa bidhaa zote zinazoshukiwa kuwa vitega uchumi wa kundi la wapiganaji wa kiislamu la al Shabab kuanzia mwezi februari mwaka uliopita, ili kuzuia wapiganaji hao wa waasi kupata fedha za kufadhili shuguhuli zao ikiwa ni pamoja na ununuzi wa silaha na kuwalipa mishahara wapiganaji wake.

Bandari hiyo ya Kismayo iko chini ya jeshi la umoja wa Afrika kwa pamoja na serikali ya Somalia tangu ilipokombolewa kutoka kwa wapiganaji wa Kiislamu wa Al Shabaab.

Jeshi la Kenya kwa sasa ndilo linalohudumu mjini Kismayo na katika maeneo kadhaa ya Kati na Kusini mwa Somalia.