AMISOM yakutana kuhusu kuchangia taarifa

Image caption Harakati za AMISOM Somalia

Ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia (Amison), kwa ushirikiano na wahisani wake, umeanza mkutano hii leo na washirika wake mjini Mombasa Pwani ya Kenya kuhusu kuchangia habari na taarifa muhimu.

Lengo la mkutano huo ni kubuni mpango utakaowezesha nchi zilizochangia wanajeshi kwa AMISOM kuchangia taarifa mara kwa mara kati ya Amisom, mashirika ya usalama nchini Somalia na mashirika mengine ya kikanda .

Mkutano huo wa siku tatu, umehudhuriwa na maafisa kutoka mashirika ya usalama nchini Somalia, viongiozi wa nchi zilizo na vikosi vyao nchini Somalia, waakilishi kutoka Ethiopia, Sudan Kusini, Mali, Chad, IGAD , AU na wengineo.

Akiongea wakati wa sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo, mjumbe maalum wa muungano wa Afrika nchini Somalia,Mahamat Saleh Annadif aliwakumbusha washirika kuwa vitendo vya kigaidi vinavyofanywa nchini humo havina mpaka.

Kwa hivyo, vita dhidi ya ugaidi lazima vifanywe kwa mpangilio unaofaa. Baada ya kukabiliwa na changamoto nyingi, kundi la Al-Shabab limeanza kubuni njia mbadala za kupambana na maadui wake kwa kukusanya taarifa za kijasusi.

Mkutano huu unatarajiwa kuangazia kwa kina hali inayokumba Somalia hususan vitendo vya kigaidi, uhalifu wa kupangwa na kuongezeka kwa idadi ya silaha ndogondogo

Pia unalenga kuimarisha miundo mbinu ili kuwezesha nchi kuchangia taarifa wakati wote pamoja na mengi mengineyo.