Vikosi vya usalama vyapelekwa Guinnea

Vikosi vya usalama vimepelekwa Kusini Mashariki mwa Guinea baada ya watu takriban 54 kuuawa katika mapigano ya kikabila.

Amri ya kutotembea ovyo tayari imetangazwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa N’Zerekore.

Mapigano hayo yalisambaa kutoka mji jirani ambapo walinzi wa jamii ya Guerze walimpiga hadi kumuua kijana wa kabila la Konianke ambaye walimtuhumu kwa wizi. Watu walioshuhudia wamesema, baadhi ya watu waliopoteza maisha katika mapigano hayo ya siku tatu walikatwakatwa kwa mapanga ama kuchomwa moto wakiwa hai.

Awali mamlaka husika iliweka idadi ya watu waliokufa kuwa ni 12, lakini idadi hiyo iliongezeka ghafla baada ya miili kuokotwa kutoka katika mitaa ya mji wa N’zerekore siku ya Jumatano.Takriban watu 130 inasemekana wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Msemaji wa serikali, Damantang Albert Camara, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba, hali ya utulivu imerejeshwa na watu 50 wamekamatwa.Ripoti za awali zinaeleza kuwa, mapigano ya hapa na pale bado yanaendelea katika maeneo ya vijijini.

Guinea ina historia ya msuguano wa makabila kati ya makundi mawili, huku mapigano yakiibuka mara kwa mara kuhusu masuala ya kidini na matatizo mengine.

Watu wa jamii ya Guerze wengi wao ni Wakristo ama wafugaji, wakati wale wa Konianke ni Waislamu wanaohusishwa kuwa karibu na watu wa kabila la Mandingo ambao wanaishi katika nchi jirani na Guinea.

Machafuko ya sasa, kwa mara ya kwanza yaliibuka Jumatatu katika kijiji cha Koule kabla ya kusambaa karibu na N’zerekore kilomita zipatazo 570 kusini mashariki mwa mji mkuu, Conakry.

Jeshi lilitangaza amri ya kutotembea ovyo katika mji huo wenye wakazi 300,000 ili kurejesha hali ya utulivu.

Siku ya Jumanne, Rais Alpha Conde, akihutubia kwa njia ya televisheni alitoa wito wa kurejeshwa kwa hali ya utulivu na umoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Septemba mwaka huu.“Mji wa N’zerekore umeshuhudia matukio yaliyosababisha upotevu wa maisha, majeruhi na uharibifu wa mali.

Kutokana na hali hiyo, natoa wito kwa wananchi kutulia”, alisema Rais Conde katika hotuba yake kwa taifa.