Siku 100 za serikali ya Kenyatta. Nini changamoto?

Image caption Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi katika mahakama ya ICC

Mgomo wa walimu, kuzorota kwa usalama na uhasama wa kikabila, ndizo zimekuwa changamoto kubwa kwa siku miamoja za serikali ya rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na muungano wake wa Jubilee.

Mgomo wa walimu wa wiki nne ambao ulisitishwa Jumatano, ulikuwa umetishia kuvuruga mpango wa masomo na zaidi mitihani ambayo inaanza wiki hii.

Mitihani hiyo ilitarajiwa kuwaanda wanafunzi kwa mitihani ya kitaifa inayoanza katika muda wa miezi miwili.

Changamoto nyingine kubwa,iliyomkabili Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto, ulikuwa mgawanyiko uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi.

Kura ya maoni zilizochapishwa mwezi huu zilionyesha kuwa asilimia 51 ya wakenya wana imani na serikali ya Kenyatta huku asilimia 48 wakiwa na imani na Bwana Ruto.

Serikali ya Kenyatta pia imekuwa na wakati mgumu kukabiliana na utovu wa usalama unaosababishwa na magenge ya wahalifu pamoja na uhasama wa kikabila.

Ingawa mauaji yamepungua katika wiki chache zilizopita, wakati mmoja Kenyatta alionya kuwa angetuma jeshi katika maeneo yaliyokuwa yanatokota kutokana na mapigano ya kikabila.

Zaidi ya watu 100 waliuawa kwenye mapiganao hayo na kutia dosari siku 100 za kwanza za utawala wa Kenyatta.

Wadadisi wa kisiasa walisema kuwa baadhi ya vurugu zilitokana na Kenyatta kuchelewa kumteua waziri wa usalama.

Licha ya serikali hiyo kuahidi kupunguza gharama ya maisha, bado hapajakuwa na juhudi za kutosha kupunguza bei za bidhaa muhimu.

Bei za bidhaa badala yake zimepanda huku wananchi wakilalamika kuwa gharama ya maisha imepanda sana chini ya utawala wa Jubilee. Kwa upande mwingine, serikali imetimiza ahadi ya kutoa huduma za uzazi bila malipo kwa wanawake kote nchini.

Licha ya kuwepo changamoto kubwa katika mpango huo ikiwemo ukosefu wa hospitali, idadi ndogo ya wauguzi , akina mama wamefurahia huduma hizo.

Serikali ya Kenyatta pia imekuwa na kibarua kigumu kudhibiti ajali za barabarani ambazo zimesababisha vifo vingi, nyingi ya ajali hizi zimesababishwa sana na polisi wa trafiki kutokuwa wakali katika kukabiliana na madereva wanaokiuka sheria za barabarani.