Umoja wa kiarabu wamuunga mkono Kerry

Umoja wa Nchi za Kiarabu umeunga mkono mpango wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bw. John Kerry, wa kuanzisha upya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Wapalestina.

Uungaji mkono huo, umekuja wakati Bw. Kerry alipokutana na wanachama wa umoja huo nchini Jordan, ikiwa ni ziara yake ya sita ya Mashariki ya Kati katika miezi ya hivi karibuni.

Mazungumzo ya mwisho ya moja kwa moja kati ya Israel na Palestina yalivunjika miaka miwili iliyopita baada ya kutoafikiana kuhusu masuala ya makaazi.

Bw. Kerry amesema, anamatumaini kwamba, pande hizo mbili hivi karibuni zitaweza kukaa meza moja ya mazungumzo.

Kumekuwa na maendeleo makubwa kati ya Israel na Palestina tangu juhudi zake kuanzisha upya mazungumzo zianze miezi kadhaa iliyopita, amesema.

''Lakini, kupitia kazi ngumu na uvumilivu na muhimu zaidi kupitia kazi ya polepole tumeweza kupunguza tofauti hizo kwa hatua kubwa,” amewaambia waandishi wa habari mjini Amman.

Hata hivyo, Bw. Kerry hakuweka ndani uwazi wa mazungumzo yake, akidai kuwa, bado kuna maeneo ambayo bado yanahitaji kufanyiwa kazi.”

Kadhalika, alitoa wito kwa Israel kuangalia kwa undani mpango wa amani wa Saudi Arabia kwanza uliopendekezwa mwaka 2002.

Mpango huo unatoa fursa ya kutambuliwa kwa taifa la Israel, lakini endapo itarejesha ardhi yote iliyopora wakati wa vita vya mwaka 1967 na kukubali kutatua tatizo la wakimbizi wa Kipalestina kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwaka 1948.

Bw. Kerry amesema, mpango huo unaipa Israel fursa ya amani na nchi za Kiarabu.

Kwa upande wake, Israel imesema, haiwezi kuukubali kama ulivyopendekezwa awali, lakini imeonyesha dalili za kuwa tayari kufikiria wazo la mpango huo.

Wajumbe wa Umoja wa Nchi za Kiarabu huko Jordan baadaye walitoa taarifa wakisema “wanaamini mawazo ya Bw. Kerry yaliyopendekezwa kwa kamati leo yamebeba msingi na mazingira mazuri ya kuanzisha majadiliano, hasa kuhusu vipengele vipya vya masuala ya siasa, uchumi, na usalama.”

Bw. Kerry ametoa kwa Wapalestina motisha za kiuchumi zenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 4 kama sehemu ya juhudi zake za kuweka mazingira ya kufanyika kwa mazungumzo ya amani.

Siku ya Jumanne, mwanadiplomasia huyo wa Marekani, alikutana na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kwa saa tano.

Mwezi uliopita Bw. Kerry alifanya mazungumzo kadhaa ya kidiplomasia yaliyowahusisha viongozi wa Palestina na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Suala la makazi ya Wayahudi katika Ukingo wa Magharibi, limebakia kuwa moja ya kikwazo kikubwa kati ya pande hizo mbili.

Bw. Abbas amesema kwamba, Israel lazima isitishe ujenzi wa makaazi hayo kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya amani yaliyokwama , wakati ambapo Bw. Netanyahu ametoa wito kwa Bw. Abbas kurejea katika mazungumzo bila ya masharti yoyote.

Mapema wiki hii, kulikuwa na hasira huko Israel, baada ya Umoja wa Ulaya kupitisha miongozi mipya inayozuia miradi ya Israel katika maeneo yanayokaliwa ya Wapalestina kupata misaada ya umoja huo ama fedha.

Jumatano, Israel iliidhinisha kwa mara ya mwisho ujenzi wa zaidi ya makazi mapya 700, huko Modiin Ilit eneo lililopo kati ya Jerusalem na Tel Aviv.

Mmoja wa maafisa wa Palestina aliyeshiriki kwenye mazungumzo na Bw. Kerry, Mohammed Ishtayeh, amesema hatua hiyo ya Israel imefanyika ili kuzuia juhudi za Bw. Kerry.

“Imekuwa ni kawaida kuona tabia hii ya Israel kila mara afisa wa Marekani ama wa kimataifa anapotembelea eneo hili kusukuma mbele mpango wa mazungumzo,” amesema Bw. Ishtayyeh.