Maafisa wa uchaguzi waachiliwa Mali

Image caption Wanajeshi wa Mali wangali wanpapambaa na waasi nchini Mali

Maafisa wa uchaguzi waliokuwa wametekwa nyara Kaskazini mwa Mali wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu wa urais wameachiliwa huru.

Maafisa wanasema kuwa wafanyakazi hao walikamatwa Jumamosi katika eneo laTessalit wakati wakitoa kadi za kupigia.

Waasi wa Tuareg wanashukiwa kuwa wao ndio waliowakamata maafisa hao.

Hivi maajuzi Mali iliondoa sheria ya hali ya hatari iliyokuwa imewekwa tangu Januari wakati ambapo Ufaransa ilipoingili kati mgogoro wa kisiasa uliokuwa unakumba taifa hilo na kukabiliana na waasi waliokuwa wameteka Kaskazini mwa nchi.

Gavana wa jimbo la Kidal Kaskazini, Adama Kamissoko, aliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wafanyakazi hao walikuwa wametekwa nyara na wapiganaji wa Tuareg.

Waliachiliwa huru Jumapili na kuchukuliwa na wanajeshi wa Ufaransa waliowapeleka katika kambi ya Jeshi ambayo haiko mbali sana na eneo la Tessalit.

Wanajeshi wa Ufaransa waliopelekwa Mali, mapema mwaka huu wako katika eneo hilo wakishirikiana na wanajeshi wa Chad ambao ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa, Minusma.

Hata hivyo idadi ya watu waliokuwa wametekwa nyara haijulikani baadhi ya ripoti zikisema kuwa ni kati ya watu wawili hadi sita.

Katika eneo la Tessalit, takriban umbali wa kilomita, 200 kutoka mji wa Kidal, maafisa wanasema kuwa naibu meya wa mji huo alikuwa mmoja wa waliokamatwa.

Inasemekana hawakujeruhiwa.

Kitendo cha kuwakamata kiliamrishwa na mmoja wa viongozi wa Tuareg wa vuguvugu la kitaifa la ukombozi wa Azawad ambaye alikamatwa na kwa sasa anahojiwa katika eneo la Tessalit,kwa mujibu wa afisaa moja ambaye hakutaka kutajwa.

Hali ya taharuki imetanda mjini Kidal kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tarahe 28 mwezi huu. Lengo la uchaguzi huo ni kurejesha utawala wa kiraia

Wapiganaji wa Tuareg wanaotaka kujitenga walihusika na uasi uliosababisha wapiganaji wa kiisilamu kudhibiti eneo la Kaskazini mwa Mali.