Maelfu wamlaki Papa Rio De Janeiro

Baba Mtakatifu Francis amelakiwa na maelfu ya mahujaji wa Brazil wakati akianza ziara yake ya kwanza ya nje tangu achaguliwe kuwa mkuu wa Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu huyo wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini alitembelea jiji la Rio De Janeiro, akiwa kwenye gari la wazi na kisha kukutana na Rais Dilma Rousseff , katika kasri la taifa la gavana.

Baada ya kuondoka, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi, kuwatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali na gharama kubwa za ziara hiyo.

Yuko Brazil kuhudhuria Sherehe za Siku ya Vijana Wakatoliki Duniani.

Katika hotuba yake mara baada ya kuwasili, Baba Mtakatifu alitoa wito kwa vijana Wakatoliki kuwa manabii wa mataifa yote.

“Nimekuja kukutana na vijana kutoka sehemu zote duniani, waliovutika kwenye mikono ya Yesu Kristo Mwokozi,” amesema akiimanisha sanamu maarufu ya Yesu iliyopo katika jiji la Rio.

“Wanataka kutafuta hifadhi katika mikono yake, karibu kabisa na moyo wake ili wasikie wito wake kwa nguvu na wazi.”

Takriban saa moja mara baada ya sherehe za kumkaribisha, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na yale ya kushtua dhidi ya waandamanaji nje ya kasri.

Yalikuwa ni maandamano ya hivi karibuni ambayo waandamanaji wanasema ni ya kupinga vitendo vilivyokithri vya rushwa ndani ya serikali na nchi nzima.

Lakini baadhi yao wamechukizwa na dola za Kimarekani milioni 53 zilizotumika kuandaa ziara ya Baba Mtakatifu.

Kulikuwa na uharibifu kiasi na watu kadhaa kukamatwa, lakini ilikuwa kama ishara kwamba, upo uwezekano wa ziara hiyo ya kihistoria ya Baba Mtakatifu ikagubikwa na matukio yasiyo ya kawaida ya kisiasa.

Katika hatua nyingine, jeshi la Brazil limesema, bomu la kutengeneza nyumbani limegunduliwa karibu na eneo moja takatifu kati ya Rio na Sao Paulo ambalo kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki anatarajiwa kulitembelea siku ya Jumatano.

Bomu hilo lilikowa na nguvu kidogo, lilidhibitiwa baada ye.

Wakati Baba Mtakatifu Francis akiteremka kutoka kwenye ndege ya shirika la Alitalia, kwenye uwanja wa ndege wa Rio, mapema Jumatatu, alilakiwa na Rais Rousseff huku umati wa watu ukishangilia na alikabidhiwa shada la maua, huku kwaya ya vijana ikiimba wimbo unaohusu siku ya vijana.

Aliwapungia mkono watu na msafara wake kuelekea katikati ya Rio ambako maelfu ya mahujaji walikuwa wamekusanyika.

Baba Mtakatifu Francis alionekana mwenye furaha na kutulia wakati akielekea jijini Rio akiwa ndani ya gari la kawaida huku dirisha likiwa limefunguliwa na maafisa usalama wakihangaika kuudhibiti umati.

Kulikuwa na matukio ya fujo wakati gari lake lilipokwama kwenye moja ya msongamano wa magari katika jiji la Rio, baada ya dereva wake kukosea njia na kuzikosa zile zilioandaliwa kwa ajili ya msafara wa Papa.

Mara umati ulizingira gari lake ukiwa na matumaini ya kumuona kwa karibu ama kumgusa. Mwanamke mmoja alimpitisha mtoto wake kwenye dirisha la gari ili Baba Mtakatifu ambusu.

Alipofika katikati ya jiji Papa alipanda gari la wazi lililoandaliwa maalum kwa ajili yake, huku akipunga mkono kwa maelfu ya watu waliojipanga pembezoni mwa barabara.

“Siwezi kusafiri kwenda Rome, lakini amekuja kuifanya nchi yangu kuwa njema na kuimarisha imani yetu,” alisema mzee mmoja wa miaka 73, Idaclea Rangel, huku akibubujikwa na machozi.

Mamlaka imeimarisha ulinzi wakati wa ziara ya siku saba ya Papa, kufuatia wiki kadhaa za maandamano nchi nzima kupinga rushwa na utawala mbovu.

Papa Francis alikataa kutumia gari maalum lisilopenyeza risasi, licha ya maombi kutoka kwa maafisa wa Brazil, maafisa wa usalama wapatao 30,000, jeshi na polisi wataimarisha ulinzi wakati wa ziara hiyo.

Zaidi ya vijana Wakatoliki milioni moja wanatarajiwa kukusanyika Rio kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani, ambyo huadhimishwa kila baada ya miaka miwili, ni sherehe za waumini Wakatoliki.

Papa huyo mzaliwa wa Argentina, ambaye alishika wadhifa huo Machi mwaka huu, anatarajiwa kuongoza ibada katika ufukwe wa pwani ya Copacabana siku ya Alhamisi na pia kutembelea moja ya vitongoji masikini.