Mashirika yahofia hali ya kibinadamu DRC

Image caption Mashirika ya misaada yanataka UN kujali hali ya raia wakati mgogoro DRC ukiendelea

Mashirika ya misaada katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo , yameelezea hofu kuhusu operesheni ya kijeshi inayopangwa na Umoja wa Mataifa yakisema kuwa itavuruga zaidi hali ya kibinadamu nchini humo.

Mashirika hayo yanayoshughulikia wakimbizi yanasema kuwa umoja wa mataifa unastahili kutumia mbinu salama zaidi ili kuwaokoa raia kutokana na athari za hatua ya kikosi cha Umoja huo kuingilia kati mzozo unaoendelea.

Umoja huo una zaidi ya wanajeshi elfu tatu.

Tayari wanajeshi wameanza kushika doria

Shirika la misaada la Medecins Sans Frontieres hapo awali lililalamika kuwa kuwepo kwa vikosi vya UN kunaweza kutatiza shughuli za shirika hilo kuwapa msaada waathiriwa wa mgogoro huo kwani huenda wakalengwa kwa mashambulizi na wapiganaji.

Baraza la umoja wa mataifa baadaye leo litajadili hali nchini DRC ambako zaidi ya watu milioni mbili unusu wameachwa bila makaazi kutokana na mzozo huo.