Maandamano yachacha Misri

Image caption Waandamanaji wamekita kambi kutaka Morsi aachiliwe

Maelfu ya wafuasi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani nchini Misri, Mohammed Morsi wameandamana usiku kucha hadi karibu na kambi moja ya kijeshi mjini Cairo kabla ya kurudi na kukita kambi kando ya msikiti mmoja.

Hata hivyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na jeshi licha ya onyo kutoka kwa waziri wa maswala ya ndani nchini humo Mohammed Ibrahim, kwamba mamlaka itajibu vitisho vyovyote dhidi ya usalama kutoka kwa waandamanaji hao.

Zaidi ya wafuasi 70 wanaotaka Morsi kurejeshwa madarakani waliuawa baada ya ghasia kuzuka kati ya waandamanaji na vikosi vya jeshi hapo Jumamosi.

Waziri wa mambo ya nje nchini humo amezitaka pande zote kwenye mgogoro huu kujizuia na kusababisha ghasia, siku moja baada ya ghasia nchini humo kusababisha vifo vya watu 70.

Kwenye mahojiano na BBC,Nabil Fahmy alisema kuwa pande zote zinapaswa kujizuia na kuchochea ghasia kwa kutumia vurugu.

Mnamo siku ya Jumamosi, wafusai wa aliyekuwa rais Morsi, walikabiliana na polisi pamoja na maafisa wengine wa usalama huku maelfu ya waandamanaji hao wakiendelea kupiga kambi.

Wakati huohuo, rais wa muda Adly Mansour amemuamuru waziri wake mkuu kulikabidhi jeshi mamlaka kuwakamata raia.

Mwandishi wa BBC Jim Muir ambaye yuko mjini Cairo anasema kuwa baadhi ya watu wanaiona hii kama dalili ya wasiwasi na mwanzo wa serikali kuanza kupambana na waandamanaji waliokita kambi katika msikiti wa Rabaa al-Adawiya .

Waziri wa mambo ya ndani, Mohamed Ibrahim amekuwa akionya mara kwa mara kuwa waandamanaji hao watatawanyishwa karibuni , ingawa waandamanaji wenyewe wanasema hawatabanduka.

Kulikuwa na ghasia siku ya Jumapili, huku watu wawili wakiuawa mjini Cairo.

Mwishoni mwa wiki wapiganaji kumi wa kiisilamu waliuawa na jeshi katika Rasi ya Sinai ambako wamezidisha mapigano kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Mena.