Ahukumiwa kifo kwa kisa cha Tebbut

Image caption Tebbut alitekwa nyara na kupelekwa Somalia baada ya mumewe kuuawa nchini Kenya

Mahakama moja nchini Kenya imemhukumu kifo mfanyakazi wa zamani wa hoteli baada ya kumpata na hatia ya kuwa miongoni mwa genge lililomuua mtalii muingereza na kisha kumteka nyara mkewe.

Jaji alimpata na hatia Ali Babito Kololo kwa kulielekeza genge hilo kwenye hoteli iliyopo katika kisiwa kimoja ambako David Tebbutt alikuwa na mkewe, Judith.

Baada ya kumuua mumewe Judith mwaka 2011, mwanamke huyo alitekwa nyara na kuzuiwa mateka nchini Somalia kwa miezi sita kabla ya kuachiwa huru.

Kololo amehukumiwa kifo lakini inadhaniwa hukumu hiyo itageuka kuwa kifungo cha maisha gerezani.Amesisitiza hana hatia na kwamba yeye pia alitekwa na watu hao waliokuwa wamejihami kwa bunduki.

Polisi wa Uingereza walisaidiana na wa Kenya kufanya uchunguzi wa kesi hiyo na kumpata na hatia Babito Kololo kwa wizi wa mabavu.

Kenya haijatekeleza hukumu ya kifo tangu mwaka 1987 na Kololo huenda akahudumia kifungo cha maisha jela.

Alikuwa amefutwa kazi katika hoteli hiyo miezi kadhaa kabla ya kuwaelekeza maharamia katika chumba walimokuwa Tebbut na mumewe katika hoteli moja kisiwani Lamu.

Alikanusha mashtaka wakati kesi yake ilipokuwa inasikilizwa mjini Lamu, akisema kuwa alilazimishwa na maharamia hao kuwaelekeza kwa mateka.

Polisi wa Uingereza walisema kuwa maafisa walisafiri kwenda Kenya kusaidia na uchunguzi wao.