UN yaamrisha M23 kusalimisha silaha

Waasi wa M23

Umoja wa Mataifa umewapa wapiganaji wa M23 walioko Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia saa 48 kusalimisha silaha, la sivyo watakabiliwa kijeshi.

Kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa cha wanajeshi 3000 kitasaidiana na jeshi la Congo kuweka eneo la usalama mjini Goma.Kikosi hicho kimekubaliwa kutumia nguvu dhidi ya waasi wanaolaumiwa kwa kuwaua raia katika maeneo karibu na mji wa Goma.

Mapema mwezi huu mapigano kati ya M23 na jeshi la Congo yalizuka mashariki mwa nchi ambapo Umoja wa Mataifa ulilaumu waasi wa M23 kwa kuwaua kiholela raia katika eneo la Mutaho viungani mwa Goma.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa umewataka waasi wote na raia walioko Mashariki mwa Congo kusalimisha silaha walizonazo katika kambi ya jeshi la Umoja wa Mataifa ifikapo Alhamisi jioni.Onyo hilo limeongeza yeyote atakayepatikana na silaha atachukuliwa kuwa mpiganaji.

Hali ya usalama imeendelea kudorora Mashariki mwa nchi na onyo la sasa linanuia kuzuia waasi dhidi ya kukaribia mji wa Goma. Takriban watu 70,000 wamekimbia makwao, kufuatia mapigano kati ya jeshi na waasi. Umoja wa Mataifa unasema Wengi wamekimbilia nchi jirani ya Uganda.