Waandamanaji nchini Misri hawatishiki

Image caption Wafuasi wa aliyekuwa rais Mohammed Morsi

Wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi -- wamekataa wito uliotolewa na wizara ya mambo ya ndani kumaliza maandamano yao katika medani mbili kubwa za mjini Cairo.

Msemaji wao Alaa Mostafa amesema maandamano yao yataendelea.

Wizara iliwataka waandamanaji kuondoka na kuwapa fursa ya kuwalinda wakati wakiondoka na ahadi ya kutowapeleka mahakamani iwapo watatii maelekezo ya wizara hiyo.

Jumatano serikali inayoungwa mkono na jeshi nchini humo iliamuru polisi kuwatawanya waandamanaji walioweka kambi katika midani hizo.

Bw. Morsi Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia aliondolewa na jeshi mwezi mmoja uliopita. Marekani imeitaka Misri kuheshimu uhuru wa kukutana ikiwemo kuweka kambi katika maeneo ya mikusanyiko.