Kura zaanza kuhesabiwa Zimbabwe

Masanduku ya kura Zimbabwe

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Zimbabwe kufuatia uchaguzi wa Urais.Idadi kubwa ya wapiga kura walijitokeza kwa uchaguzi huo ambapo kuna, ushandani mkali kati ya Rais Robert Mugabe wa Zanu-PF na Waziri Mkuu Morgan Tvsangirai wa MDC.

Waangalizi wa Muungano wa Afrika wamesema uchaguzi huo ulifanyika kwa amani japo chama cha MDC kimelalamikia dosari kwenye daftari ya wapiga kura.

Matokeo yanatarajiwa kutangazwa kwa muda wa siku tano. Rais Mugabe wa miaka 89 amesema atastaafu baada ya kuwa madarakani kwa miaka 33 ikiwa atashindwa katika uchaguzi huo.Polisi nchini Zimbabwe wameonya kuwakamata wote watakaojaribu kutangaza matokeo yasiyo kweli.

Vyama vya MDC na Zanu-PF vimekuwa kwenye serikali ya muungano tangu mwaka wa 2009 baada ya kuafikia muafaka wa kumaliza ghasia za kisiasa.Muda wa kupiga kura uliongezwa hadi jioni kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura waliojitokeza.

Mshindi lazima apate asili mia 50 ya kura. Ikiwa hakuna mshindi wa moja kwa moja raundi ya pili ya uchaguzi itakua Septemba 11.Uchaguzi wa Zimbabwe ni wa kwanza chini ya katiba mpya iliyopitishwa mwezi Machi mwaka huu.