Kenya yafutilia mbali leseni za madini

Image caption Makampuni ya madini inadaiwa kuafikia mikataba na serikali kwa njia ya siri

Serikali ya Kenya imefutilia mbali leseni zote za uchimbaji wa madini ambazo ilikuwa imetoa kwa makampuni ya uchimbaji katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu.

Waziri wa madini Najib Balala, alisema kuwa serikali iliyopita ya Rais Mwai Kibaki iliafikia mikataba kwa haraka sana na makampuni ya uchumbaji bila ya kuzingatia uwazi katika kutoa kandarasi za uchimbaji.

Pia alimfuta kazi kamishna wa madini (Moses Masibo). Wiki jana shirika la fedha duniani IMF lilielezea wasiwasi kuhusu mikataba ambayo serikali ya Kenya ilikuwa imeafikia na makampuni ya uchimbaji likisema ilifanywa kwa usiri mkubwa.

Kenya hivi karibuni iligundua sehemu kadhaa za nchi zenye madini kama vile titanium, copper na niobium inayopsemekana kuwa na thamani ya mabilioni ya dola.