Wanajeshi 23 mahakamani Congo Brazaville

Mahakama katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville imeanza kusikiliza kesi dhidi ya wanajeshi 23 walioshtakiwa kwa kosa la kusababisha mlipuko katika ghala la silaha mjini humo.

Zaidi ya watu miambili walifariki na wengine elfu mbili miatatu kujeruhiwa kwenye milipuko hiyo mwezi Machi mwaka jana.

Milipuko ilisikika umbali wa kilomita nyingi katika nchi jirani ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo na kuharibu madirisha na paa za nyumba mjini Kinshasa. Wanajeshi hao wameshtakiwa kwa kosa la kuanzisha moto ulioteketeza bohari hilo kwa maksudi.

Majaji kadhaa waliapishwa siku ya Ijumaa ili kusikiliza kesi hiyo ambayo wanajeshi 20 wanashitakiwa pia kwa kosa la kutishia usalama wa nchi.

Milipuko hiyo iliharibu nyumba nyingi na kuwaacha zaidi ya watu 17,000 bila makao.

Uchunguzi katika kesi hiyo ulisababisha kukamatwa kwa watu 26 akiwemo naibu mkuu wa baraza la usalama wa kitaifa ingawa raia watatu waliokuwa wamekamatwa waliachiliwa.

Kwa mujibu wa taarifa za gazeti pekee linalochapishwa kila siku, Les Depeches de Brazzaville, lilinukuu taarifa iliyosema kuwa vikao vya kusikilizwa kwa kesi hiyo vitapeperushwa moja kwa moja katika baadhi ya vituo vya redio na televisheni.