Baraza la jiji lamuomba radhi Mandela

Image caption Mandela amekuwa akiugua kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa akiwa amelazwa hospitalini

Maafisa wakuu mjini Johannesburg, wamemuomba radhi Nelson Mandela kwa kumtumia kimakosa hati ya kudai malipo pamoja na onyo kuwa huenda akakatiwa huduma ya maji na stima kwa kuchelewa kulipia huduma hizo.

Walisema kuwa onyo hilo linalomtaka Mandela alipe dola 660 la sivyo akatiwe huduma hizo ilipaswa kutumwa kwa mtu mwingine wala sio Mandela.

Maafisa wa baraza la jiji wamekuwa wakipokea malalamiko mengi kutoka kwa wakaazi kuhusu hati za madai ya malipo ya huduma wanazopokea kutoka kwa baraza la jiji.

Mandela amekuwa hospitalini tangu tarehe 8 mwezi Juni akitibiwa homa ya mapafu.

"baraza la jiji lingependa kuomba radhi familia ya Mandela kwa kwa athari zozote zilizotokana na jambo hili,''

Notisi ya baraza la jiji ilitishia kukomesha huduma hizo na hata kuchukua hatua za kisheria ikiwa deni hilo la siku 30 halingelipwa.

Hata hivyo, msemaji wa baraza hilo Kgamanyane Maphologela alielezea kuwa anwani na nambari ya akaunti ya kulipia zilikuwa za mteja mwingine ambaye ni jirani wa Mandela.

Vile vile nambari ya barabara na jina la mteja zilikuwa sawa , ila mteja anaishi katika sehemu tofauti.

Bwana Maphologela alisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wale waliofanya kosa hilo.

Familia ya Mandela, ambayo makaazi yake yako katika mtaa wa kifahari wa Houghton, daima hutembelewa na watu wenye nia ya kuiafriji familia ya Mandela, kumtakia afya njema rais huyo wa zamani.

Mwezi jana makao makuu ya chama cha kitaifa cha ANC, inasemekana kilipokea kimakosa hati za kudaiwa randi milioni 3.5.

Mandela ambaye ni rais wa kwanza wa Afrika Kusini kuchaguliwa kidemokrasia, anatazamiwa na wengi kama baba wa taifa.

Aidha Mandela alifungwa jela kwa miaka 27 baada ya kuanzisha harakati dhidi ya uliokuwa utawala wa kibaguzi.