Wahamiaji wapata afueni Italy

Image caption Maelfu ya wahamiaji haramu kuingia nchini Malta

Meli iliyokuwa imewabeba wahamiaji 102 waliookolewa inaelekea nchini Italy baada ya Rome kukubali kuwaruhusu wahamiaji hao kuingia nchini humo na hivyo kumaliza hali ya suitofahamu iliyokuwepo kati ya wamiliki wa meli hiyo na maafisa wa Malta

Waziri mkuu wa Malta Joseph Muscat aliishukuru serikali ya Italia kwa kusema kuwa uamuzi huo utaimarisha uhusiano kati ya nchi hizo.

Malta ilikataa shinikizo za Muungano wa Ulaya kuwaruhusu wahamiaji hao kuingia nchini humo ikisisitiza kuwa meli iliyokuwa imewabeba iwarejeshe Libya.

Ilisisitiza kuwa kuwaruhusu waingine nchini humo ingeweza kutoa taswira mbaya kwa wahamiaji haramu.

Kisiwa hicho kidogo hupokea maelfu ya wahamiaji haramu wanaoelekea Ulaya kila mwaka .

Meli ya mafuta iliyokuwa imewabeba wahamiaji hao kutoka Libya ikielekea Malta ilikuwa inaelekea katika bandari ya Syracuse Jumatano asubuhi kulingana na maafisa wa trafiki baharini.

Kulingana na jarida la Times nchini Malta, kikundi kipya cha wahamiaji 86 kiliwasili nchini humo Jumatano asubuhi,baada ya kuokolewa ufuoni.

Tume ya Ulaya iliambia Malta siku ya Jumanne kuwa ina jukumu la kuwakubali wahamiaji hao ambao miongoni mwao kulikuwa mwanamke aliyekuwa amejeruhiwa , wanawake wanne wajawazito, na mtoto mwenye miezi mitano kwa msingi ya ubinadamu.