Syria yakana msafara wa Asaad umeshambuliwa

Image caption Bashar Al Asaad

Syria imekanusha ripoti za mashambulio dhidi ya msafara wa rais Bashar al-Assad alipokuwa akielekea msikitini Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu Damascus kuhudhuria ibada ya sherehe za Idd Il Fitr zinazokamilisha mwezi mtukufu wa Ramadhani .

Wanaharakati na wakaazi wa eneo hilo walisema kuwa mabomu kadhaa yalianguka katika eneo hilo , na taarifa kutoka upande wa waasi wa Free Syrian Army zinasema kuwa msafara wake ulishambuliwa.

Televisheni ya taifa nchini Syria ilionyesha picha za video za rais Assad akitabasamu , huku akisalimiana na maafisa alipowasili katika msikiti kwa ajili ya kushiriki sala ya Idd .

Huku baadhi ya watu waliotoa maoni yao kwenye mtandao wa Tweeter wakishuku kuwa picha hizo zilirekodiwa kabla , ni dhahiri hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa bwana Assad alipata madhara yoyote.

Waziri wake wa mawasiliano , amekanusha vikali taarifa za shambulio dhidi ya msafara wa rais akitaja shutuma hizo kama ''ndoto'' .

Amesema kuwa Bwana Assad aliendesha gari lake mwenyewe kuelekea kwenye msikiti na kila kitu kilikuwa katika hali ya kawaida.

Lakini baadhi ya wanajeshi katika jeshi la Syria walisema kuwa makombora yalirushwa katika eneo alikokuwa wakati huo yakilenga msafara wake .

Wakazi wa eneo hilo pia waliunga mkono madai hayo wakisema walisikia milio ya milipuko mapema asubuhi.

Kwa vyovyote vile yaelekea bwana Assad amenusurika .

Hii ni mara ya tatu kwa bwana Assad kuonekana hadharani katika kipindi cha wiki moja, jambo ambalo lisingeweza kufanyika miezi kadhaa iliyopita wakati mji mkuu Damascus ulipokuwa ukishambuliwa mara kwa mara