Polisi matatani kwa kula hongo Nigeria

Image caption Ni kawaida kwa polisi wa Trafiki Nigeria kula hongo barabarani

Polisi mmoja nchini Nigeria, amefutwa kazi baada ya kunaswa kwa filamu akipokea hongo ya dola 150 kutoka kwa mwenye gari aliyedaiwa kukiuka sheria za barabarani.

Filamu hiyo ilinaswa kisiri katika barabara kuu mjini Lagos, na ilitazamwa na watu wengi sana kwenye mtandao wa YouTube na imechezwa sana pia kwenye vituo vya runinga kote nchini humo.

Kwenye filamu hiyo, Sajenti Chris Omeleze anasema kuwa yeye ni sehemu ya mtandao mkubwa wa maafisa wenye kula hongo barabarani.

Lakini poliisi nchini Nigeria wanasisitiza kuwa sivyo. Chris alifutwa kazi chini ya siku moja baada ya kanda hiyo ya video kuonekana.

Duru zinasema kuwa polisi wa trafiki huchukua hongo kutoka kwa wanaokiuka sheria za barabarani sio nadra.

Hata hivyo ni nadra kwa washukiwa wa Kitendo hicho kukamatwa.

Kanda hiyo iliyotizamwa na watu zaidi ya laki moja kwenye YouTube inaonyesha Sagenti Omeleze akiwa ndani ya gari akimtaka dereva ampe hongo la sivyo amchukulie hatua.

Kanda hiyo ilitolewa siku ya Jumanne huku msemaji wa polisi akithibitisha kuwa sajenti Omeleze alifutwa kazi baadaye.

Hata hivyo msemaji wa polisi alisisitiza kuwa Sgt Omeleze alikuwa anafanya hivyo akiwa peke yake na alijidai kumpigia simu mwenzake kumhadaa dereva ili aweze kutoa pesa kwa haraka.