Marekani yatahadhari nchini Pakistan

Image caption Ubalozi wa Marekani nchini Pakistan

Serikali ya Marekani imewaagiza wafanyikazi wake wasio husika na maswala ya dharura kuondoka katika afisi yake ya ubalozi katika mji wa Lahore nchini Pakistan. Afisa mmoja nchini Marekani anasema amri hiyo ilitolewa kutokana na tishio la shambulio la kigaidi katika afisi za ujumbe wake.

Wizara ya mambo ya nje imeiambia BBC kuwa imewaagiza maafisa ambao hawana shughuli za dharura kuondoka katika ubalozi wake wa Lahore na kusema kuwa kuna taarifa za kuaminika kuhusu tisho la kushambulia ubalozi huo.

Kadhalika Marekani imewaonya raiya wake kutosafiri Pakistan bila dharura.

Hata hivyo hadi sasa Pakistan haikuwa imeorodheshwa na Marekani katika balozi zinazotakiwa kufungwa tangu Jumapili iliyopita kwa hofu ya kushambuliwa na wapiganaji. Sasa Pakistan imechukua tahadhari kubwa.

Milipuko ya mabomu imewaua zaidi ya watu 40 katika siku mbili zilizopita.

Katika jiji la Magharibi la Quetta, ambako watu thelathini waliuawa na mshambuliaji wa bomu wa kujitolea kufa, tisa kati yao walifariki asubuhi hii baada ya watu wasiojulikana kuwafyatulia watu risasi msikitini katika sherehe za Eid.

Watu watano wamekamatwa kuhusiana na shambulio hilo.