Waandamanaji wa Morsi kutawanywa leo

Image caption Wafuasi wa Morsi waahidi kuendelea na maandamano

Wafuasi wa Rais aliyeondolewa mamlakani, Mohammed Morsi, wameendelea kupiga kambi katika sehemu mbili kuu za mji mkuu Cairo, licha ya maafisa wakuu kuahidi kuanza kuwafurusha waandamanaji hao.

Kulingana na Taarifa hizo shughuli hiyo itaanza pole pole ambapo maafisa wa usalama watawazuia wafuasi zaidi kuingia katika maeneo hayo mawili .

Oparesheni ya kutaka kuwatimua maelfu ya wafuasi hao inatarajiwa kuanza muda mfupi kuanzia sasa.

Maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Morsi, huku wakipeperusha bendera ya Misri na kubeba mabango yenye picha za Morsi.

Duru kutoka wizara ya mambo ya ndani zimeambia BBC kuwa maafisa wa usalama wanajiandaa kuziba maeneo waliyopiga kambi wafuasi hao, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kuwatawanya waandamanaji hao.

Vuguvugu la Muslim Brotherhood lilitoa taarifa siku ya Jumapili ambayo ilionekana kuwataka wafuasi wao kuunda kambi mbadala za muda ikiwa watafurushwa kutoka maeneo hayo yaliyokaribu na msikiti.