Maelfu wahamishwa kwa nguvu Lagos

Image caption Lagos una takriban watu milioni 15

Melfu ya watu nchini Nigeria wanaishi kwa hofu ya kuondolewa katika makaazi yao kama sehemu ya mradi wa serikali wa maendeleo mjini Lagos.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.

Shirika hilo limesema kuwa karibu watu 9,000 tayari wamelazimishwa kuondoka makwao katika sehemu ya kwanza ya mradi huu.

"athari za watu kuondolewa makwao kwa lazima zimekuwa mbaya sana," alisema afisaa wa shirika hilo Oluwatosin Popoola.

Afisaa mwingine aliambia BBC kuwa watu walioachwa bila makao watakuwa wa kwanza kupata nyumba pindi ujenzi wa nyumba mpya utakapokamilika.

Mitaa duni imekuwa ikipanuka mjini Lagos kutokana na msongamano wa watu wanaotafuta ajira mjini humo.

Amnesty imechapisha picha za Satelite zikionyesha kile inachosema ni eneo lililokuwa na watu wengi na ambalo sasa limebaki vifusi baada ya kuporomoshwa Februari mwaka huu.

Shirikia hilo linasema kuwa lililazimika kupiga picha hizo ili kupinga madai ya serikali kuwa eneo lililoathirika lilikuwa jaa la taka.

Kwa mujibu wa shirika hilo, wenyeji sasa wanalala nje wakikabiliwa na tisho la kuambukizwa magonjwa, kuvamiwa na wezi na kuwa maelfu wamepoteza njia zao za kujikimu kimaisha.

Ripoti ya shirika hilo inataka utawala wa Lagos kusitisha mpango wa kuwafurusha watu kwa lazima.

Inaarifiwa kuwa ni changamoto kubwa sana kwa serikali kuuweka mji huo kuwa sawa kimiundo msingi kwa ajili ya idadi kubwa ya watu wanaoishi hapo, ikikisiwa kuwa zaidi ya milioni 15.

Wakosoaji wanasema kuwa pengo kati ya matajiri na maskini linavyoendelea kuwa pana, wale waliaochwa bila makao wanasalia kuwa na ndoto tu ya kuwahi kumiliki nyumba katika nyumba mpya zinazojengwa ili kuondoa mitaa ya mabanda kwenye mji huo.

Mwanamke mmjoa aliyefurushwa aliambia BBC kuwa alienda kwa serikali za mitaa kutafuta msaada lakini hatarajii kama atapata msaada wowote.

Kamishna wa nyumba mjini Lagos aliambia BBC kuwa serikali inajaribu kadri ya uwezo wake kuboresha maisha ya watu wa jimbo hilo.