Balaa Misri: zaidi ya 15 wauwa

Image caption Maandamano nchini Misri

Zaidi ya watu kumi na watano wameripotiwa kuuwawa wakati maafisa wa usalama nchini Misri walipoanza operesheni ya kuwatimua wafuasi wa rais aliyeng'olewa madarakani Mohammed Morsi, waliokuwa wamekita kambi mjini Cairo.

Lakini vuguvugu la Undugu wa Kiislamu, Muslim Brotherhood, ambalo linaunga mkono maandamano hayo limesema idadi ya waliouwawa inazidi kumi na watano.

Milipuko ya risasi ilisikika na magari ya kivita yametumika kuwatimua waandamanaji hao.

Maafisa wa usalama walifyatua gesi ya kutoa machozi.

Maafisa wamesema kuwa kambi ya waandamanaji hao katika Medani ya Nahda magharibi mwa mji wa Cairo imevunjwa na waandamanaji kutawanywa.

Wizara ya mambo ya ndani imesema kuwa operesheni ya kusafisha barabara za mji huo inaendelea. Wanaharakati wanaomuunga mkono bwana Morsi walifukuzwa hadi hifadhi ya wanyama pori iliyopo karibu pamoja na chuo kikuu cha Cairo, kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali Nile TV kimesema.