MSF - Heri tuondoke Somalia

Image caption mkuu wa shirika la MSF Dr. Unni Karunakara

Shirika la kutoa misaada la Madaktari wasiokuwa na Mipaka, Medicins Sans Frontieres limetangaza kusitisha shuguli zake zote nchini Somalia.

Akitangaza uamuzi huo, mkuu wa shirika hilo Dr. Unni Karunakara amesema kuwa MSF imelazimika kuondoka nchini Somalia baada ya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wafanyikazi wake.

Shirika hilo limekuwa likitoa misaada nchini Somalia tangu mwaka 1991. Dr. Kaunakara amesema kuwa uamuzi huu umekuwa mgumu zaidi kuchukua. Amelalamika kuwa wafanyikazi wao wamelazimika kufanya kazi katika mazingira hatari huku wapiganaji na baadhi ya viongozi wamekuwa wakichangia, kufadhili au kuunga mkono kwa njia moja au nyingine mashambulio dhidi ya mashirika ya misaada.

Katika kukiri kuwa hatua hiyo ina athari kubwa, Dr. Karunakara amesema kuwa wale watakao umia zaidi ni raia wa kawaida. Tangu shirika hilo lianze kuhudu nchini Somalia wafanyikazi wake 16 wameuawa katika mashambulio. Wengine wawili kutoka Uhispania walitekwa nyara na kuzuiliwa kwa takriban miaka miwili kabl aya kuachiliwa mwezi Julai.