al shabaab wapora MSF Somalia

Image caption Mkuu wa MSF Unni Karunakara.

Ripoti kutoka Somalia zinasema kuwa wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa kiislamu la al Shabab wameanza kupora kliniki zinazomilikiwa na shirika la kutoa msaada wa kitabibu la Medicins Sans Frontiers, MSF, baada ya shirika hilo kutangaza kuwa linajiondoa kutoka nchini humo.

Wenyeji katika eneo la Bay kusini magharibi wamesema waliona wanamgambo wakipora madawa, kompyuta pamoja na mitambo mingine kutoka katika makao makuu ya shirika hilo.

Siku ya jumatano, shirika la MSF lilisema kuwa linasitisha shughuli zake zote kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya wafanyikazi wake.

Tangu shirika hilo lianze kufanya kazi nchini Somalia mwaka 1991, wafanyikazi wake kumi na sita wameuwawa.

Wengine wawili walitekwanyara mwaka 2011 na kuachiliwa hivi maajuzi.