Magenge yafanya shule kufungwa Afrika kusini

Image caption Mji wa Maneberg ambako shule 16 zimefungwa

Ongezeko la fujo na ghasia za magenge imesababisha maafisa wa elimu nchini Afrika kusini kufunga kwa siku mbili shule 16 katika jimbo la Magharibi la Cape.

Angalau watu 50 wameripotiwa kujeruhiwa au kuuwawa baada ya kupigwa risasi katika eneo la Manenberg katika siku za hivi karibuni.

Waziri Mkuu katika jimbo hilo Bi Helen Zille ameiomba serikali kuu kuepeka jeshi katika eneo hilo kwani polisi wameshindwa kukabiliana na fujo hizo za magenge.

Msimamizi katika shule mmoja eno hilo alifariki baada ya kupigwa risasa wiki moja iliyopita.

Uamuzi wa kufunga shule ulichukuliwa baada ya walimu kulalamika kwamba wanahofia maisha yao.

Bi Aysha Ismail, ambaye ni mama ya mmoja wa waathiriwa alisema kuna haja ya polisi zaidi kuweko katika eneo hilo la Manenberg,ili kupunguza visa vya utovu wa usalama.

Mama huyo alisema mtoto wake wa kiume alipigwa risasi katika mahali ambapo kwa kawaida watoto hucheza kila siku. Marafiki zake wanasema kijana huyo alikuwa mwanachama wa genge linalojulikana kama Amerika na ambalo linahangaisha watu sana eneo hilo.