Mubarak kuachiwa huru kwa dhamana

Image caption Hosni Mubarak

Mahakama nchini Misri inatarajia kutoa uamuzi wa ama kumuachia huru kwa dhamana au la, Rais wa zamani nchi hiyo Hosni Mubarak.

Bwana Mubarak anakabiliwa na mashtaka ya rushwa ambayo yamemfanya asalie rumande bila dhamana.

Rais huyo wa zamani wa Misri mwenye umri wa miaka 85 pia anakabili kesi nyingine ya kushirikiana katika mauji ya waandamanaji wakati wa vuguvugu la mapinduzi ya kiraia yaliyomuondoa madarakani mwaka 2011.

Wakati huo huo, Mawaziri wa mambo ya nje na masuala ya kigeni wa nchi za umoja wa Ulaya wanakutana kujadili hatima ya Misri, huku wengine watarajia kufuta kabisa misaada yote kwa taifa hilo lililopo kwenye hali tata kwa sasa.

Baadhi ya mawaziri wameomba fungu la msaada wa Yuro bilioni 5 sawa na dola Bilioni 6.7 wanalopewa Misri kufutwa baada ya watu zaidi ya 900 kuuwawa kwenye ghasia tangu wiki iliyopita.

Vifo hivyo vimetokea mara baada ya serikali ya mpito kuamuru vikosi vya polisi na jeshi kufunga kambi mbili za wafuasi wa rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Morsi.

Vyanzo vya habari vya mwandishi wa BBC mjini Brussels, Matthew Price vinasema mawaziri hao wanakusudia kusitisha misaada ya kijeshi na usalama inayotolewa na nchi mbalimbali za ulaya kwa taifa la Misri.

Mkurugenzi wa sera kwenye umoja wa Ulaya,Baroness Catherine Ashton ameomba kufanya suluhisho la kisiasa nchini Misri na ana imani ya kujenga matumaini ya kufanyika hilo baina ya serikali ya mpito na chama cha Muslim Brotherhood.

Nako nchini Marekani maofisa wakuu wa serikali ya Obama wamekuwa katika mkutano wa dharura mjini Washington kujadili iwapo waendelee kutoa msaada wa dola bilioni 1.3 kwa serikali ya Misri.

Mamia ya wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood wameuawa ndani ya wiki moja na Marekani imeonya kuwa kukosa kuijumuisha Muslim Brotherhood katika suluhisho la kisiasa la nchi hiyo, kutaathiri msaada unaotolewa, ambao mwingi unaenda kwa jeshi.

UCHELEWESHWAJI UNATARAJIWA

Bwana Mubarak 85,alishitakiwa mwezi Juni mwaka 2012 kwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya waandamanaji mwaka 2011 na kufungwa kifungo cha maisha jela.

Lakini mwezi Januari 2013 alishinda rufaa aliyokata na mahakama ya rufaa kuamuru kesi yake isikilizwe upya.

Kesi hiyo ilianza upya mwezi Mei 2013,lakini bwana Mubarak tayari amekwishakaa kizuizini kupita muda ambao unatakiwa kwa mashtaka hayo.

Wakili wa Mubarak , Fareed Al Dib amesema anatarajia mteja wake ataachiliwa huru baada ya amri ya mahakama na atasalia na kesi za mashitaka dhidi ya rushwa pekee.

Licha ya upande wa mashitaka kutarajiwa kupinga kwa kukata rufaa dhidi ya kuachiwa kwake,jambo ambalo litachelewesha kutoka kwake gerezani.

Kesi hiyo pia inahusiana na tuhuma za rais huyo kupokea hongo kama zawadi kutoka kwa gazeti la serikali Al-Ahram.

Mwandishi wa BBC mjini Cairo anasema familia ya Mubarak imelipa gharama zote na zawadi ambazo anadaiwa kuzichukua, suala ambalo linamuongezea matumaini wakili wake kuwa huenda mteja wake akaachiliwa huru.

Hukumu ya rufaa itasomwa kwenye gereza ambalo Mubaraq amefungwa.

Wadadisi wanasema iwapo Mubarak ataachiliwa, hiyo itarudisha hisia za wengi za kwamba jeshi linataka kurejesha utawala ambao uliondolewa kwa mapinduzi ya kiraia ya mwaka 2011,

Suala ambalo huenda likarudisha maandamano makubwa na ghasia zaidi kuendelea kuzuka nchini humo.