UN yataka uchunguzi kufanywa Syria

Image caption Maandamano Syria juu ya silaha za kemikali

Baraza la usalama la umoja wa mataifa limefanya kikao cha dharura kujadili madai kwamba wanajeshi wa serikali ya Syria wametumia silaha za kemikali pale walipofanya shambulio dhidi ya eneo lililopo nje kidogo ya mji mkuu wa Damascus hapo jana jumatano.

Wanaharakati wa upinzani wamesema kuwa mamia ya watu wakiwemo watoto wameuwawa huku muungano wa upinzani ukiyataja mauaji hayo ya halaiki. Serikali ya Syria imekanusha kwamba imetumia silaha hizo.

Mwenyekiti wa baraza la usalama, Maria Parceval, ambaye ni balozi wa Argentinean katika umoja wa mataifa amesema kuwa wanachama wa baraza hilo wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na madai hayo.

"Naweza kusema kuwa kuna wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanachama wa baraza kuhusu madai hayo. Kuna hisia kwamba kuna haja ya kuwa wazi kuhusu kilichotokea na hali kufuatiliwa kwa makini,'' anasema Bi. Maria Parceval.

''Wanachama wote wanakubaliana kwamba matumizi yoyote ya silaha za kemikali, kwa yeyote katika mzozo huu, na katika mazingira yoyote ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Kulikuwa pia na makubaliano ya kutoa wito wa kusitishwa uhasama na vita.''

Kadhalika Bi. Perceval amesema kuwa kulikuwa na makubaliano kuhusu haja ya kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusiana na swala hilo.

''Wanachama wa baraza la usalama wametaka katibu mkuu aingilie kati ili kuhakikisha kuwa uchunguzi wa haraka na wa kina usioegemea upande wowote unafanywa. Wanachama wa baraza wameelezea haja ya kutolewa mara moja msaada wa kibinadamu kwa waathiriwa. Hatimaye baraza la usalama limetoa rambi rambi kwa waathiriwa pamoja na familia zao,'' ameongeza kusema Bi. Maria Perceval, mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.