Umoja wa mataifa washambulia M23 Goma

Image caption Wapiganaji wa kundi la M23

Vikosi vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameshambulia maeneo yanayoshikiliwa na waasi karibu na mji wa Mashariki wa Goma..

Umoja wa Mataifa ulikua unajibu mashambulio ya mizinga ya waasi wa kundi la M23 katika mji wa Goma mnamo siku ya Alhamisi,amesema msemaji wa Umoja wa mataifa.

Maafisa wa Congo wanasema raia watano waliuwawa katika mji huo.

Msemaji wa M23 ameiambia BBC kwamba hawakuushambulia mji huo na kulishtumu jeshi kwa kuchochea mapambano.

Kikosi kipya cha umoja wa mataifa kimetumwa katika eneo hilo kupambana na waasi kina idhini ya kuwatenga na kuwapokonya silaha waasi.

Wanajeshi wake 3,000 wanajiunga na jeshi la kuweka amani la Umoja wa Mataifa,Monusco lenye wanajeshi 18,000 wakipewa jukumu la kuwalinda raia.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Luteni-Kanali Felix-Prosper Basse amesema helikopta mbili za Umoja wa Mataifa zilihusika katika mashambulio hayo ya hivi karibuni,wakisaidiwa na jeshi la Congo, wakishambulia maeneo ya waasi katika Kibati masafa ya kilometa15 kaskazini ya Goma.

"Mapigano yameingia awamu mpya wakati Monusco sasa inapambana na waasi wakishirikiana na vikosi vya serikali ," amekiambia kipindi cha BBC cha Focus on Africa.

Vikosi vya Umoja wa Mataifa vilikua vinahifadhi maeneo hayo kwa kuwa waasi wamekua wakiwashambulia ovyo raia, alisema.

Mnamo mwezi wa November, waasi wa M23 waliuteka kwa muda mfupi mji wa Goma, unaopakana na Rwanda, wakiondoka baada tu ya kukubaliana masharti kadhaa mkiwemo kujadiliana na serikali.

Waziri wa habari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ,Lambert Mende ameaiambia Idhaa ya Maziwa Makuu ya BBC kwamba baadhi ya makombora yaliyoangukia Goma mnamo siku ya Alhamisi kutokea eneo la Rwanda.

Raia watano waliofariki katika mashambulio hayo ya mizinga ni pamoja na watoto na mwanamke mmoja, alisema.

Rwanda imekanusha mara kwa mara madai ya Umoja wa Mataifa kwamba imekua ikiwaunga mkono waaasi wa M23.

Kama wengi wa viongozi wa Rwanda wapiganaji wengi wa M23 ni kutoka jamii ya Watutsi.

Waliasi kutoka jeshi la Congo mnamo Aprili 2012,na kulazimisha takriban watu laki 8 kuhama makaazi yao katika machafuko yaliyozuka katika eneo hili lenye utajiri mkubwa wa maadini.

Mazungumzo ya kutafuta amani katika Uganda mwaka huu yaliyokusudiwa kutanzua manungu'niko yao yamekwama.