Watu 20 wauawa nchini Nigeria

Image caption Wapiganaji wa Boko Haram nchini Nigeria

Watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram wamewauwa takriban watu ishirini wanachama wa makundi kadhaa ya ulinzi waliokuwa wakipinga kundi hilo Kaskazini mwa jimbo la Borno.

Wakuu wa jeshi la nchi hiyo wanasema vifo hivyo vilitokea katika mashambulio mawili tofauti siku ya Jumapili na Jumatatu.

Kundi hilo la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulio nchini Nigeria tangu mwaka wa 2009.

Mwezi Mei mwaka huu, rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan, alitangaza hali ya hatari katika majimbo matatu ta Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, akisema kundi hilo la Boko Haram linahatarisha usalama wa taifa hilo.

Jeshi la nchi hiyo lilianzisha operesheni kali ya kuwasaka wapiganaji wa kundi hilo, ambalo linataka kuundwa kwa taifa huru litakalozingatia sheria za Kiislamu maarufu kwama Sharia.

Jeshi la nchi hiyo lilihimiza wakaazi wa majimbo hayo kuunnda makundi ya raia ili kukabiliana na kundi hilo endapo watawavamia.

Lakini kwa sasa kundi hilo la Boko Haram, linaonekana linalipiza kisasi dhidi ya makundi hayo ya kiraia na hivyo kuongeza wasi wasi kuwa kuundwa kwa makundi hayo huenda kukachochea ghasia zaidi nchini humo.

Siku ya Jumapili, watu waliokuwa na sare rasmi za jeshi la nchi hiyo walivamia mkutano wa kundi moja la ulinzi wa kiraia na kuwafyatulia risasi na kuwauawa watu kumi na wanne.

Afisa mmoja wa serikali ya nchi hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu wengine wanne waliuawa kwenye shambulio lingine siku ya Jumatatu usiku katika kijiji cha Borno, wilayani Damasak.

Wapiganaji hao waliwashambulia wanachama wa kundi lingine linalojiita jeshi la wanainchi au Civilian Joint Task Force wakiwa usingizini katika hoteli moja.