Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji DRC

Image caption Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Congo

Umoja wa Mataifa umeanzisha uchunguzi kufuatia madai kuwa wanajeshi wake waliwauwa raia wawili wa Congo, wakati wa maandamano mjini Goma, Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku mapigano na waasi yakiendelea.

Walioshuhudia tukio hilo wameliambia shirika la habari ya AFP, kuwa watu wawili waliuawa siku ya Jumamosi wakati umati wa wati ulipojaribu kuvamia kituo kimoja cha jeshi hilo la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa wanajeshi wake kutoka Uruguay waliafyatulia risasi.

Serikali ya Uruguay imekanusha madai hayo na kuelekezea lawama maafisa wa polisi wa Congo.

Kikosi kipya cha Umoja wa Mataifa kimetumwa katika eneo hilo kukabiliana na waasi.

Wiki iliyopita wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa walishambulia maeneo kadhaa yanayothibitiwa na waasi karibu na mji huo wa Goma.

Hata hivyo hakuna taarifa yoyote rasmi kuhusu idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa kwenye mapigano hayo.

Daktari mmoja katika eneo hilo ameliambia shirika la Habari la AP kuwa aliona miili ta watu themanini na wawili waliouawa, ishirini na watatu kati yao wakiwa wanajeshi wa serikali.