Mtu anayedaiwa kuharibu mabango ya rais Mugabe aachiliwa huru

Image caption Wafuasi wa rais Mugabe

Mahakama moja nchini Zimbabwe imemuachilia huru mtu mmoja ambaye alifunguliwa mashtaka ya kutaka kutumia mabango ya kampeini ya rais Robert Mugabe, kama makaratasi ya kufuta uchafu, katika baa yake.

Waendesha mashtaka nchini humo walidai kuwa Takura Mufumisi, mwenye umri wa miaka 26, alikiuka sheria za uchaguzi kwa kuharibu makaratasi ya kampeini.

Lakini wakili wa mshukiwa huyo amesema mahakama iliamuru kuwa waendesha mashtaka walishindwa kuthibitisha madai dhidi ya mteja wake.

Rais Mugabe, 89, alishinda awamu yake ya saba kuwa rais wa Zimbabwe baada ya kumshinda mpinzani wake mkuu, Morgan Tsvangirai, katika uchaguzi uliofanyika tarehe thelathini na moja Julai mwaka huu.

Bwana Tsvangirai, hata hivyo amepinga ushindi huo na kudai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Mufumisi alikamatwa katika baa yake katika mji wa Kusini wa Masvingo, wiki moja kabla ya uchaguzi huo.

Wakili wa mshukiwa huyo amesema hakimu alimuachilia huru kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

''Serikali ilikuwa na shahidi mmoja pekee, ambaye aliiambia mahakama hiyo kuwa alimuona tu mshukiwa akiwa msalani'' Alisema wakili huyo.

Mufumisi aliachiliwa huru tarehe tano Agosti, lakini kesi yake imeangaziwa tu wikii hii na kuzua mjadala mkali miongoni mwa raia wa nchi hiyo.

Wakili mwingine, Kumbirai Mafunda, amesema idadi ya watu wanaomtusi rais Robert Mugabe imeongezeka sana katika siku za hivi karibuni.

Mwezi machi mwaka huu, afisa mmoja mwandamizi wa chama cha Movement for Demokratic Change MDC, Solomon Madzore, alikamatwa kwa madai ya kumuita rais Mugabe '' Nyani mlemavu'' katika mkutano wa kampeini ya chama hicho.

Hata hivyo afisa huyo alikanusha madai ya kutumia lugha ya matusi dhidi ya rais Mugabe.