Ethiopia yakana kukandamiza upinzani

Image caption Zaidi ya watu elfu moja walihudhuia mkutano wa hadhara wa watu wanopinga siasa kali nchini humo

Takriban wanachama 100 wa chama cha upinzani cha Semayawi nchini Ethiopia walikamatwa na wengine kuchapwa vibaya sana mwishoni mwa wiki. Hii ni kwa mujibu wa chama hicho.

Mwenyekiti wa chama hicho Yilekal Getachew alisema kuwa vifaa kama vipaza sauti vilinaswa kabla ya mkutano wa hadhara uliokuwa umepangiwa kufanyika Jumapili kuharamishwa.

Waziri wa habari na mawasiliano Shimeles Kemal alikanusha madai kuwa polisi walifanya msako kuwakamata waandamanaji hao.

Serikali ilisema kuwa sehemu kulikoandaliwa mkutano wa hadhara, ilikuwa imewekewa kikundi cha wanachama wa vuguvugu linalopinga siasa kali.

Chama tawala EPRDF kinasifika kwa kuweka sheria kalu sana kudhibiti maisha ya watu kukutana hadharani

Maandamano ya umma yaliandaliwa mwezi Juni na yalikuwa ya kwanza makubwa kwenye barabara za mji mkuu Addis Ababa tangu mwaka 2005 wakati mamia ya waandamanaji walipouawa wakati wakiandamana.

Maandamano hayo yalifanyika kutoa wito wa kuachiliwa kwa waandishi wa habari na wanaharakati waliokamatwa.

Aidha yale yaliyokuwa yemeitishwa siku ya Jumapili, yalikuwa ya kushinikiza mageuzi ya kisiasa.

Aidha bwana Shimeles alisema kuwa kikundi chochote kilichotaka kuandaa mkutano wa hadhara lazima kiombe idhini ya serikali.

Alisema kuwa maafisa wa utawala hawawezi kukataa kutoa kibali cha kufanya maandamano lakini akasisitiza kuwa mkutano wao ufanyike katika sehemu tofauti

Hailemariam Desalegn alichukua wadhifa wa waziri mkuu mwaka mmoja uliopita kufuatia kifo cha hayati Meles Zenawi.

Ethiopia ni mwandani wa Marekani katika kukabiliana na harakati za wapiganaji wa kiisilamu katika eneo hilo.