Mwanawe al-Senussi atekwa nyara Libya

Image caption Sanussi alikuwa mshirika mkubwa sana wa Gaddafi

Mwana wa kike wa aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini Libya , ametekwa nyara baada ya kuondoka jela mjini Tripoli.

Waziri wa sheria Salah al-Marghani alisema kuwa polisi walikuwa wanamsindikiza Anoud Abdullah al-Senussi kutoka jela Jumatatu mchana wakati walipovamiwa na genge lililokuwa limejihami kwa silaha.

Aliongeza kuwa watekaji nyara waliwafyatulia risasi polisi kabla ya kumteka nyara Bi Senussi.

Bi Senussi alikuwa emekamilisha kifungo chake cha miezi kumi kwa kuingia Libya kutumia stakabadhi bandia mwezi Oktoba mwaka jana.

Alikamatwa baada ya kurejea Libya kumtembelea babake Abdullah al-Senussi, ambaye yuko jela.

Babake anazuiliwa kwa madai ya kuhusika na uhalifu uliotendwa wakati wa utawala wa Muammar Gaddafi.

Pia anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya (ICC),ambayo inamtuhumu kwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa harakati zilizoiangusha iliyokuwa serikali ya Gaddafi mwaka 2011.

Maafisa wa polisi waliokuwa wanamsindikiza bi Senussi kuelekea uwanja wa ndege wa Tripoli akiwa na jamaa zake kuelekea Kusini mwa mji wa Sebha wakati msafara wa magari waliokuwa nao ulipovamiwa.

Bwana Marghani ameomba watu kutoa maelezo yoyote waliyonayo kuhusu utekaji nyara huo.

Katika miezi ya hivi karibuni , aliweza kuruhusiwa kumtembelea babake.

Mwandishi wa BBC Rana Jawad alisema kuwa tukio la hivi karibuni huenda likaiweka nguvu dhana kuwa Libya haiko tayari kuwachukulia hatua vigogo waliohusika na uhalifu ikiwemo Abdullah al-Senussi na Saif Gaddafi, wote wanaotakikana na mahakama ya ICC.