Zaidi ya milioni mbili watoroka Syria

Image caption UNHCR linasema kuwa watoto ndio wengi wanaotoroka vita Syria

Shirika la umoja wa matafa linalowashughulikia wakimbizi limesema kuwa limewasajili zaidi ya wakimbizi milioni mbili kutokana na mzozo wa Syria hii ikiwa idadi maradufu ya hali ilivyokuwa miezi sita iliyopita. Idadi hii ya wakimbizi imeongezeka kwa wakimbizi milioni moja

Takriban wengine laki saba wametoroka na kuingia Lebanon huku raia wa Syria waliotoroka makwao wakiwa wengi kuliko wananchi wenye uraia mwingine kote duniani.

Mkuu wa shirika hilo , Antonio Guterres, ameiambia BBC kuwa waathiriwa hao wa ghasia wanaishi maisha mabaya na wanahitaji msaada wa dharura.

Ufaransa imetoa ripoti yake ya ujasusi inayosema kuwa Serikali ya Syria ilitumia kemikali nyingi katika shambulizi lililofanyika katika viunga vya jiji kuu la Damascus mwezi uliopita.

Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa viongozi wa bunge na waziri mkuu , Jean-Marc Ayrault. Nchi hiyo ikishirikiana na Marekani zinataka hatua za kijeshi kuchukuliwa dhidi ya Syria.

Mjumbe wa umoja wa mataifa Syria ameonya kuwa ghasia zinazoendelea zitaitumbukiza nchini hiyo katika mauaji ya halaiki.

Mokhtar Lamani ameiambia BBC kuwa mashambulizi ya makundi mbalimbali yanatisha halikadhalika watu wengi kuhama katika vijiji kwa kuzingatia ikiwa ni wasuni, waalawite ama wakristo.

Duru zinasema kuwa Rais Barak Obama huenda anapanga kuchukua hatua kali na kubwa zaidi za kijeshi dhidi ya Syria kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.

Habari hizi zimejitokeza wakati wanasiasa wakuu wakijiandaa kuwasilisha ombi lao kwa kamati ya bunge la Congress kutaka kuuungwa mkono kuhusu pendekezo la kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria.

Ripoti ya Umoja wa mataifa ilisema kuwa idfadi kubwa ya wanawake , watoto na wanume wanatoroka wakikimbilia mameneo ya mipakani wakiwa tu na nguo chake walizobeba migongoni mwao.

Nusu ya wale wanaotoroka ni watoto , kulingana na shirika la UNHCR huku zaidi ya thuluthi moja wakiwa chini ya umri wa miaka 11.

Ni watoto 118,000 wakimbizi pekee wameweza kuendelea na masomo yao huku zaidi ya nusu wakipokea ushauri nasaha. Pamoja na hilo kuna wasiwasi kuwa watoto hawa hawana uelewa wowote kuhusu watakavyoijenga upya nchi yao katika siku za usoni.