Ligi ya Uingereza yavunja rekodi

Image caption Mkufunzio wa Arsenal Arsene Wenger

Vilabu vya ligi kuu ya Uingereza vimetumia pauni milioni 630 katika kipindi kilichokamilika cha kuwasajili wachezaji wapya kutoka vilabu vingine, kulingana na kitengo kinachohusika na maswala ya biashara ya michezo katika kampuni ya Deloitte.

Rekodi ya awali ilikuwa pauni milioni 500 iliyowekwa mwaka 2008. Kipindi cha wachezaji kuruhusiwa kuhama kutoka vilabu fulani na kusajiliwa kwengineko, kilifika kikomo hapo jana siku ya Jumatatu .

Miongoni mwa wachezaji waliogharimu mamilioni ya pauni ni mchezaji Mesut Ozil aliyehama kutoka Real Madrid na kuelekea Arsenal kwa kima cha pauni milioni 42.4.

Manchester United ilimsajili Marouane Fellaini kwa pauni milioni 27.5 kutoka Everton.

"kisa cha msimu huu wa wachezaji kuhama ni kuwa rekodi imevunjwa , msimu huu mamilioni imetumiwa kuliko katika msimu mwingine wowote katika historia ya Ligi ya Uingereza,'' alisema Dan Jones wa Deloitte.

Hata hivyo mchezaji Gareth Bale, alihamia Real Madrid kutoka Tottenham Hotspur kwa kima cha pauni milioni 85.

Vilabu hivyo sasa viko na pesa nyingi sana kutokana na mikataba iliyotiwa saini kati ya vilabu ya televisheni za uingereza kupeperusha mechi zao.

Mfano BT imelipa pauni milioni 738 kwa kipindi cha miaka mitatu kuweza kupeperusha mechi moja kwa moja kutoka viwanjani wakati televisheini ya Sky ikilipa pauni bilioni 2.3 kupeperusha mechi 116 msimu huu.

Ingawa ligi zengine ulaya hazijfikia utumaiji wa pesa kwenye ligi ya Uingereza, zimetumia mamilioni katika kuwanunua wachezaji kutoka vilabu vingine