Mkutano wa G20 waanza Syria ikitokota

Image caption Urusi ndio mwenyeji wa mkutano wa G20

Viongozi wa mataifa wanachama wa kundi la G20 wanakusanyika katika mji wa St Petersburg nchini Urusi kwa mkutano wao wa kila mwaka wa mataifa ishirini yenye ustawi mkubwa wa kiviwanda duniani.

Duru zinasema maswala ya kiuchumi huenda yakafumbiwa macho katika mkutano huo kutokana na mzozo uliopo nchini Syria na tofauti zilizopo kati ya Marekani na Urusi kuhusu mipango ya kuishambulia Syria kwa madai ya kutumia silaha za kemikali.

Rais Barack Obama anasema kuwa dunia haiwezi kuepuka tendo la kutochukua hatua dhidi ya Serikali ya Syria.

Naye Rais Vladimir Putin amesema kuwa Marekani ikishambulia Syria litakuwa tendo la uchokozi. Rais wa Marekani ameeleza kwamba Serikali ya Syria imekaidi marufuku ya kimataifa ya kutumia silaha za kemikali na hatua inapaswa kuchukuliwa.

Kiongozi wa Urusi anasema vingine kuwa Marekani kushambulia Syria bila idhini ya Umoja wa Mataifa ni kukiuka sheria ya kimataifa.

Hapa hali ya maoni mawili yanayohitiliafiana kutoka kwa Marais wawili maarufu.

Inaonekana kuwa tofauti kubwa inayohusu Syria huenda ikapata nafasi bora katika vyombo vya habari kuliko mkutano unaoendelea wa mataifa tajiri zaidi duniani ya G20. Marais hawa wawili ni wanachama wa G20 ambapo watataka kushawishi mataifa kuunga mkono upande wao.