Rooney awajibu wakosoaji wake

Image caption Jeraha alilopata Rooney

Wayne Rooney amechapisha picha ya jeraha alilopata kichwani baada ya wakosoaji wake kuhoji kujitolea kwake kuchezea timu ya taifa.

Rooney alijeruhiwa na mchezaji mwenzake wa Manchester United Phil Jones,kwa kumkanyaga kichwani na hivyo kumlazimisha kukaa nje ya mechi za England kufuzu kushiriki kombe la dunia zitakazochezwa Uijumaa na Jumanne.

Alisema kuwa baadhi ya watu wanaonekana kuhoji kujitolea kwake na kusema kuwa amejiondoa kwenye miuchuano ya kufuzu kwa kombe la dunia.

"nina uhakika watu wataona kwa nini sitaweza kucheza.''

Rooney, mwenye umri wa miaka 27, aliongeza kuwa hakuna sababu inayoweza kumzuia kuwasaidia wachezaji wenzake kuweza kufuzu kwa kombe la dunia.

Kocha mkuu wa Man United David Moyes alisema kuwa Rooney huenda asicheze kwa wiki tatu kutokana na jeraha alilopata Jumamosi kabla ya timu hiyo kushindwa na Liverpool, mechi ambayo Rooney hakuweza kucheza kutokana na jeraha.

Mchezaji mwenzake wa timu ya taifa Theo Walcott ameelezea kutishwa na picha hiyo akisema inafanana na picha zinazoonekana tu kwenye filamu.

Rooney ni mmoja wa wachezaji watatu ambao wamejiondoa kutoka kwenye kikosi cha timu ya taifa kwa sababu ya jeraha alilopata.

Wengine ni Glen Johnson na Jones.