Wanawake wa Botswana kurithi mali

Image caption Wanawake wa Botswana hadi leo hawakuwa na haki ya kurithi

Mahakama nchini Botswana imeweka historia kwa kusema kuwa wanawake wana haki ya kurithi chini ya sheria za kitamaduni na kukataa utamaduni wa wanaume kuwa warithi wa pekee.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa jarida moja la nchini humo Maravi Post.

Katika kesi iliyowasilishwa kwenye mahakama ya rufaa, mjini Gaborone, hoja nzito ilikuwa ikiwa wasichana waruhusiwe kurithi mali ya familia chini ya sheria za kitamaduni ambayo imekuwa ikisisitiza kuwa ni wanaume pekee walio na haki ya kurithi.

Edith Mmusi, mwenye umri wa miaka 80 aliyewasilisha kesi mahakanai ,aliteta kuwa tangu aishi katika nyumba yao yeye na dada zake wameekeza sana katika nyumba ile kuifanya iwe nzuri zaidi kwa hivyo wote wana haki ya kuirithi.

Madai yake yalipingwa na mpwa wake aliyesema kuwa kama mwanaume kwenye boma hilo yeye ndiye anayepaswa kuirithi licha ya kuwa hakuwahi kuishi katika nyumba hiyo kwani babake alipewa nyumba hiyo na jamaa mwanamume.

Majaji walipuuza historia ya sheria za kitamaduni zinazowapendelea wanaume na kuamua kuwa Edith na dada zake waweze kurithi nyumba hiyo.

"uamuzi wa mahakama ulikuwa wazi kuwa wanawake sio raia wa daraja ya chini nchini Botswana."

Baadhi ya watu walikuwa wanahofia kuwa mahakama ya rufaa ingepuuza wanawake hao na kukandamiza zaidi haki za wanawake. Lakini badala yake waliamua kwa misingi ya usawa wa kijinsia na kukataa ubaguzi wa kijinsia.

Huu bila shaka ulikuwa uamuzi muhimu sana sio tu nchini Botswana bali kwa kanda nzima ya Afrika Kusini.

Majaji walizungumzia mabadiliko katika jamii katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kwenye hukumu yao na hata kupingana na utamaduni ambao walisema unawakandamiza wanawake pamoja na kuwa umepitwa na wakati.