Kesi dhidi ya Ruto kuanza leo ICC

Image caption Naibu rais William Ruto akiondoka Kenya kuelekea Hague kwa kesi inayomkabili

Kesi dhidi ya naibu rais wa Kenya William Ruto itaanza hii leo katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC , Hague Uholanzi.

Bwana Ruto na Rais Uhuru Kenyatta, wanatuhumiwa kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 - madai anayoyakanusha.

Majaji wa mahakama hiyo wameelezea kuwa kesi hizo mbili huenda zikafanyika wakati tofauti katika kipindi chja wiki nne kila mmoja wala sio kwa wakati mmoja kama ilivyokuwa imepangwa zisikilizwe kwa wakati mmoja.

Hii ni kutokana na ombi la rais Kenyatta kuwa washukiwa hao hawapaswi kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja kwani kutakuwa na pengo la uongozi.

Duru zinasema kuwa hii bila shaka ndiyo kesi yenye utata mkubwa zaidi kuwahi kusikilizwa katika historia ya mahakama ya ICC.

Kesi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi Novemba.

Ghasia hizo ambazo zilizuka baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kupinga ushindi wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, watu 1,300 walifariki.