Ruto: Ana kwa ana na ICC

Image caption Naibu rais wa Kenya na wafuasi wake alipokuwa anaelekea ICC

Kesi dhidi ya naibu rais wa Kenya William Ruto imeanza kusikilizwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC , Hague Uholanzi.

Bwana Ruto na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na mwandishi wa habari Joshua Arap Sang, wanatuhumiwa kwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 - madai ambayo wanayakanusha.

Majaji wa mahakama hiyo wameelezea kuwa kesi hizo mbili huenda zikafanyika nyakati tofauti katika kipindi cha wiki nne kila mmoja, wala sio kwa wakati mmoja kama ilivyokuwa imepangwa awali .

Hii ni kutokana na ombi la rais Kenyatta kuwa washukiwa hao hawapaswi kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja kwani kutakuwa na pengo la uongozi.

Duru zinasema kuwa hii bila shaka ndiyo kesi yenye utata mkubwa zaidi kuwahi kusikilizwa katika historia ya mahakama ya ICC.

Kesi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi Novemba.

Ghasia hizo ambazo zilizuka baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kupinga ushindi wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, zilisababisha vifo vya watu 1,300.

Lakini je ilikuwaje hadi kesi za washukiwa wa Kenya kufika Hague?

Baadaye Ruto na Kenyatta waliunda muungano walioutumia kugombea uongozi kwenye uchaguzi wa Machi mwaka 2013

Kesi dhidi ya Rais Kenyatta itaanza Novemba 10

Mkataba wa amani uliosaidia kumalizika kwa ghasia hizo, pia ulipendekeza kuwa wale waliohusika na ghasia wachukuliwe hatua za kisheria.

Tume iliyoongozwa na jaji Waki ambayo ilikuwa na jukumu la kuchunguza ghasia hizo, ilipendekeza kuwa ikiwa juhudi za kuunda mahakama ambayo ingesikiliza kesi hizo Kenya zingefaulu, basi kesi hizo kesi zisingepelekwe Hague.

Image caption Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008

Bwana Ruto ni afisa wa kwanza mkuu serikalini kufika mbele ya mahakama hiyo.

Mshukiwa mwingine Joshua arap Sang, pia ameshtakiwa kwa kuchochea ghasia na kusaidia katika kupanga mashambulizi dhidi ya kabila hasimu.

Mashtaka dhidi ya watatu hoa, Ruto, Kenyatta na Sang yanatokana na ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Mnamo siku ya Alhamisi, bunge la Kenya lilitoa wito wa Kenya kujiondoa kwenye mahakama hiyo ya kimataifa . Bunge lilikubali kujadili hoja hiyo.

Mahakama ilisema kuwa kesi zitaendelea, hata ikiwa Kenya itajiondoa kwenye mkataba wa Roma uliounda mahakama ya ICC

Aidha mahakama ya ICC ilianzishwa mwaka 2002 ili kusikiliza kesi za kimataifa za mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu.