Vingozi wa dini watoa Fatwa kwa Al Shabaab

Image caption Wapiganaji wa kiisilamu al shabaab

Takriban viongozi 160 wa kidini nchini Somalia wametoa kauli au Fatwa inayolaani kundi la al-Shabab, wakisema kuwa kundi hilo haliruhusiwi kabisa katika dini ya kiisilamu.

Wadadisi wanasema kuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi wa kidini nchini Somalia kutoa Fatwa aina hiyokulaani kundi hilo ambalo linadhibiti maeneo mengi ya vijijini na mijini.

Katika kongamano kuhusu tatizo la itikadi kali mjini Mogadishu, wasomi hao walisema kuwa wanalaani jambo la Al Shabaab kutumia ghasia kuwahangaisha wananchi.

Al-Shabab, au Vijana kwa maana nyingine, wanapigania kile wanachosema ni taifa la kiisilamu.

Licha ya kuondoshwa katika maeneo ya mijini katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kundi hilo bado linadhibiti miji midogo na sehemu kubwa ya vijijini.

Wakati huohuo, wenyeji wa maeneo ambako kundi hilo liko mfano mjini Bula Burte, wamesema kuwa limemuua kijana mmoja kwa kufanya uhalifu na kumkata mikono yote kijana mmoja mbele ya umati mkubwa wa watu.

Moja ya malengo ya kongamano hilo ilikuwa kuonyesha ikiwa kundi hilo lina uhalali wowote katika dini ya kiisilamu huku viongozi hao wakikubaliana kwa pamoja kuwa kundi hilo ni haramu na kinyume na dini ya kiisilamu.

''Ni kama genge linalokuja pamoja kuwaua wasomali, bila sababu yoyote kubwa,'' aliongeza msomi huyo wa kiisilamu ambaye alikwenda Somalia kutoka Marekani kushiriki kwenye kongamano hilo.

"kitu pekee wanachokitaka ni kusababisha vurugu nchini humu ili waweze kuiendeleza ajenda yao, '' alisema msomi mwingine kutoka ghuba la uwajemi.

Rais Hassan Sheikh Mohamud ndiye alifungua rasmi kongamano hilo ambalo liliwavutia wasomi wasomali kutoka kote duniani.

Aliingia mamlakani mwaka mmoja uliopita katika mpango uliofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kuona kuwa vurugu za miaka mingi zinakwisha nchini humo

Wiki jana al-Shabab walitumia akaunti yao ya Twitter kudai kuwa walivamia msururu wa magari yake.