Syria kujiunga na UN kupinga silaha za kemikali

Image caption Rais Assad anadai kuwa waasi ndio waliotumia silaha za kemikali wala sio serikali yake

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuwa umepokea nyaraka kutoka kwa Syria kuhusu kutaka kujiunga na mkataba kuhusu zana za kemikali , ambao unaharamisha utengezaji na utumiaji wa zana hizo.

Rais wa nchi hiyo,Bashar al-Assad awali aliambia kituo cha runinga cha Urusi kuwa stakabadhi hizo zinatumwa kwa UN na kuwa itawasilisha data kuhusu zana hizo mwezi mmoja baada ya kusaini mkataba huo.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na Urusi, wanajiandaa kukutana mjini Geneva kujadili mpango uliopendekezwa na Urusi mapema wiki hii.

Marekani inatuhumu serikai ya Syria kuua watu kwa kutumia silaha za kemikali

Serikali inakanusha madai hayo ikisema kuwa inawalaumu waasi kwa mashambulizi ya silaha za kemikali katika kitongoji cha Ghouta karibu na mji wa Damascus, mnamo tarehe 21 mwezi Agosti

Hatua ya Urusi na Marekani kutuma wajumbe mjini Geneva, ikiwemo maafisa wa kijeshi na maafisa wa usalama, inaonyesha kuwa pande hizo mbili zingependa sana kutumia fursa hii mwafaka, kuzungumzia swala la Syria.

Lakini vikwazo ni vingi. Marekani pamoja na Uingereza na Ufaransa, wanataka kuona hatua zikichukuliwa kumuadhibu Assad kwa makali aliyotumia dhidi ya raia wake.

Urusi imesema hili halikubaliki. Rais Putin, alieleza hasira yake kuhusu wazo la Marekani katika jarida la New York Times, akiwaonya wamarekani dhidi ya athari za nchi yao kushambulia Syria.

Ilisema kuwa visa vya ugaidi vingeendelea kukithiri.