Amnesty:Watu wahamishwa kwa nguvu Mogadishu

Image caption Wakimbizi wa ndani nchini Somalia

Maelfu ya watu wanaondoshwa kwa nguvu kutoka kutoka kambi za muda mjini Mogadishu kutoa nafasi kwa maafisa wa mji huo kufanya shughuli za usafi na ukarabati.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la Amnesty.

Shirika hilo limesema kuwa watu wameendelea kuondoshwa kwa nguvu, katika miezi ya hivi karibuni licha ya maafisa wa serikali kukosa kupata maeneo mbadala salama ambako watu hao wanaweza kuhamia.

“Hili halipaswi kuwa linafanyika kwa watu waliotoroka mji mkuu wakitafuta usalama tena kuhamishwa mkwa nguvu.

Hali hii imesababisha visa vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Serikali ina wajibu wa kulinda watu hawa wasiojiweza na kuhakikisha usalama wao,’’ alisema Gemma Davies, mtafiti mkuu wa shirika hilo la Amnesty International.

Zaidi ya watu 300,000 wanaishi katika kambi za muda mjini Mogadishu ambako wanajihifadhi kutokana na ukame, njaa na vita vya miaka mingi nchini Somalia ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Mnamo mwezi Januari, mwaka 2013, serikali ya Somalia, ilitangaza mpango wa kuwahamisha maelfu ya wakimbizi wa ndani kutoka Mogadishu katika kambi zilizo nje ya mji ili kutoa nafasi kwa ukarabati wa mji huo.

Mpango wa serikali hata hivyo ulionekana kuwa na dosari ikizingatiwa shughuli yenyewe ya kuwahamisha wakimbizi hao, muda na eneo salama ambalo wangepelekwa.