UN:Syria ilitumia silaha za kemikali

Image caption Silaha za kemikali zilitumiwa katika kitongoji kimoja cha Damscus mwezi jana

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inayotarajiwa kutolewa wiki ijayo, itathibitisha kuwa silaha za kemikali au sumu zilitumiwa nchini Syria mwezi jana, kwa mujibu wa Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa.

Hata hivyo Ban Ki-moon hakuzungumzia kuhusu ni nani aliyetumia silaha hizo kwa mashambulizi ya Agosti 21 katika kitongoji cha Ghouta mjini Damascus, kwa sababu hiyo siyo sehemu ya itakachosema ripoti hiyo.

Lakini alisema kuwa rais wa Syria Bashar Al-Assad ana hatia ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na Urusi wanaendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa kuifanya Syria kuwa salama kutokana na silaha za kemikali.

Msemaji wa waziri wa mambo ya nje wa Urusi alisema kuwa mazungumzo na mwenzake wa Marekani yangeendelea hadi usiku akisema kuwa wanaangalia kwa kina njia za kudhibiti kabisa silaha hizo.

Marekani na washirika wake wanatuhumu serikali ya Syria kwa kutumia zana za kimekali dhidi ya raia wake mwezi jana , lakini serikali imekanusha madai hayo na kuwalaumu waasi.

Bwana Ban amesema kuwa ripoti hiyo itathibitisha kwa kina kuwa silaha za kemikali zilitumiwa nchini Syria