Mashahidi 4 wajiondoa katika kesi ICC

Image caption Fatou Bensouda akiongea na waandishi wa habari ICC

Kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC, Fatou Bensouda, amepata pigo jengine baada ya mashahidi wengine wanne kujiondoa katika kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto na mshtakiwa mwenzake Joshua Arap Sang.

Hili limetokesa siku moja tu kabla ya Bensouda kuanza kuwasilisha mashahidi mbele ya mahakama siku ya Jumanne kesi dhidi ya Ruto itakapoanza tena.

Mashahidi hao wanajumuisha manusura wa moto ulioteketeza kanisa la Kiambaa mkoa wa Rift Valley na kusababisha vifo vya watu 35 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2007-2008

Bwana Ruto anatuhumiwa kwa kuchochea ghasia ili kujinufaisha kisiasa wakati Sang akidaiwa kumsaidia Ruto kuafikia malengo yake kwa kutumia kituo cha Redio alichokuwa anafanyia kazi wakati wa ghasia hizo.

Hii sio mara ya kwanza kwa mashahidi kujiondoa katika kesi dhidi ya washukiwa hawa. Wiki mbili zilizopita mashahidi wengine wawili walijitokeza nchini Kenya wakidai kuwa wanalazimishwa na upande wa Mashtaka kutoa ushahidi wa uongo dhidi ya wawili hao.

Wadadisi wanasema kuwa kujiondoa kwa mashahidi katika kesi hii bila shaka kutaathiri uwezo wa kiongozi wa Mashtaka Fatou Bensouda lakini amewahi kusikika akisema kuwa kwa mashahidi kujiondoa katika kesi yake dhidi ya Ruto na Sang sio hoja.

Kesi dhidi ya Ruto iliakhirishwa wiki jana baada ya upande wa mashtaka kusema kuwa hawajakuwa tayari kuwasilisha mashahidi wao na hivyo kupewa muda na mahakama hadi siku ya Jumanne wiki hii.