MDC yasusia ufunguzi wa bunge Zimbabwe

Image caption Mugabe amekuwa mamlakani tangu taifa hilo kujikomboa kutoka kwa mkoloni 1980

Chama rasmi cha upinzani nchini Zimbabwe, kimesusia hafla ya ufunguzi wa vikao vipya vya bunge iliyoongozwa na rais Robert Mugabe.

Chama cha MDC kimekuwa kikilalamika na kusema kuwa uchaguzi wa Mugabe uliofanyika tarehe 31 Julai, haukuwa halali.

Chama hicho kimesema kuwa ushindi wa mgombea wake Morgan Tsvangirai, uliibwa na chama tawala, madai ambayo Mugabe anakana.

Uchaguzi huo ndio ulikuwa mwisho wa serikali ya mseto iliyoongozwa na viongozi hao wawili baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata mwaka 2008.

'Ari mpya'

Uchaguzi huo hata hivyo ulifanywa kwa njia ya amani, kinyume na hali iliyoshuhudiwa katika uchaguzi uliokumbwa na ghasia pamoja na vitisho.

Bwana Mugabe, 89, alishinda asilimia 61 ya kura zilizopigwa huku Tsvangirai akipata asilimia 34.

Mugabe amesema chama chake kiko tayari kushirikiana na wanasiasa wasio waunga mkono.

Chama chake cha Zanu-PF kilishinda thuluthi moja ya viti vya bunge.

MDC kilipinga matokeo ya uchaguzi na kusema kuwa ulikumbwa na wizi wa kura.

"hana haki ya kufungua bunge na hatuwezi kushiriki katika hafla hiyo inayoongozwa naye, '' kinara wa chama cha MDC Innocent Gonese alinukuliwa akisema.

Bwana Mugabe hata hivyo hakuzungumzia chama cha MDC wakati wa hotuba yake.

Wakati huohuo, Rais Robert Mugabe, ameahidi kuendelea na mpango wa kutaifisha makampuni yanayomilikiwa na wageni baada ya kusema kuwa mpango huo utafuatiliwa kwa ari mpya.

Sheria hiyo iliyoidhinishwa kwanza mwaka 2010, inahitaji makampuni ya kigeni kutoa asilimia 50 ya hisa zake kwa raia wa Zimbabwe. Wakosoaji wanasema itaathiri uwekezaji wa nchi za nje.

Sheria hiyo mpaka sasa imetumika katika sekta ya uchimbaji migodi.