Moyes:Rooney anaweza kuwa bingwa

Image caption Rooney alirejea uwanjani baada ya jeraha alilopata kichwani na sasa anasema yuko katika hali nzuri

Mkufunzi wa klabu ya Manchester United, David Moyes, amemwambia mchezaji Wayne Rooney kuwa anaweza kuwa mchezaji mzuri zaidi kuwahi kuchezea klabu hiyo na kumtaka asalie Old Trafford wakati wa kipindi cha uhamisho.

Rooney, mwenye umri wa miaka 27, amekuwa mchezaji wa nne katika historia ya klabu hiyo kuingiza mabao 200 wakati wa mechi yao dhidi ya Leverkusen Jumanne waliposhinda kwa mabao 4-2.

Walikuwa wanashiriki mechi za kufuzu kwa michuano ya klabu bingwa barani Ulaya ingawa ndio awamu ya kwanza tu.

Wengi walisema kuwa Rooney alikuwa anatarajiwa kuhamia klabu ya Chelsea.

"tumemfahamisha hilo kuwa ana uwezo mkubwa wa kuwa bingwa wa kuingiza magoli katika Manchester United,'' alisema Moyes.

Wachezaji wengine walioingiza mabao mengi wakiwa wachezaji wa Man U ni pamoja na Sir Bobby Charlton aliyeingiza mabao 249 katika mechi, 758. Denis Law aliingiza mabao 237, Jack Rowley 211 na Wayne Rooney 200 katika mechi 402.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya England, alikuwa fahari ya wachezaji wenzake walipowashinda kwa urahisi wageni wao kutoka Ujerumani. Mabao yaliingizwa na Robin van Persie na Antonio Valencia pamoja na Rooney aliyeingiza mabao mawili.

"Wayne Rooney anaweza kujipa umaarufu sawa na wa wachezaji waliokuwa kabla yake na ambao walisifika kwa mabao yao,'' aliongeza Moyes.

"Ikiwa ataendelea kucheza hivi, basi ataweza kujipa nafasi hiyo. Alicheza vyema, vyema sana.''

Rooney bila shaka atajitahidi kuwapongeza mashabiki wao ambao daima huwashabikia kila wanapocheza.