Syria:Waasi walitumia silaha za kemikali

Image caption Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria

Mkaguzi Mkuu wa silaha katika Umoja wa Mataifa, ameambia BBC kwamba itakua vigumu kutafuta na kuziharibu silaha zote za kemikali zinazomikiliwa na utawala wa Syria.

Ake Sellstrom aliyeongoza uchunguzi ndani ya Syria mwezi jana amesema ripoti yao iliyodhihirisha utumizi wa kemikali ya sumu huenda ipelekea utawala wa Syria kuahidi kusalimisha silaha zote za sumu.

Wakati huo huo Urusi imewalaumu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kwa kutoa ripoti inayosema imeegemea upande mmoja.

Urusi inasema inayo ripoti yake inayoonyesha kwamba waasi ndio walishambulia raia kwa silaha za kemikali na siyo majeshi ya serikali. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ryabkov aliyefanya ziara mjini Damascus jana usiku amesema amepokea ushahidi wake kutoka kwa serikali ya Syria.

Amesema atawasilisha ripoti hiyo kwa wataalamu wa Urusi. Bw Ryabkov ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kutozuru maeneo ambayo Urusi ilidai waasi walitumia silaha za kemikali.

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa walipata kwamba kemikali yenye sumu ya Sarin ilitumika kuwashambulia raia viungani mwa mji wa Damascus.