Iran yataka mwafaka kuhusu Nuklia yake

Image caption Mpango wa nuklia wa Iran

Rais wa Iran, Hassan Rouhani anasema kuwa anataka kuafikia mwafaka na viongozi wa dunia kuhusu mpango wa nuklia wa nchi hiyo katika kipindi cha miezi mitatu hadi sita.

Aliambia jarida la Washington Post kuwa aliona uwezekano wa kupata suluhu kuhusu swala hilo kama hatua ya mwanzo katika kulegeza uhusiano kati ya Marekani na Iran.

Bwana Rouhani alisema kwamba anazungumza kwa idhini ya kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Khamenei, kuona kuwa swala hilo linatatuliwa.

Hii leo, Iran itafanya mazungumzo na kikundi cha P5+1 cha viongozi wa dunia, kuhusu mpango wa Iran wa kurutubisha madini ya Uranium.

Katika tukio la kipekee la maafisa wa Iran kukutana na wale wa Marekani, waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif atakutana na mwenzake wa Marekani John Kerry pamoja na wanadiplomasia kutoka Uingereza, Ufaransa, Urusi , China na Ujerumani mjini New York.

Mnamo siku ya Jumanne, Rouhani aliambia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa yuko tayari kushauriana kuhusu muda na matokeo ya mazungumzo kuhusiana na mpango wake wa Nuklia.

Iran imekuwa ikishauriana na wanachama wa kudumu wa baraza la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani tangu mwaka 2006 kuhusu mpango wake wa Nuklia.

Rais Rouhani alisema kuwa baada ya mazungumzo kuhusu mpango wake wa Nuklia , mambo yatakuwa sawa katika hatua za kusonga mbele. Aliongeza kuwa hakuna kisichowezekana.